DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA


Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425







PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.







TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Gazeti la kila siku la Mwananchi la jana, Jumanne, Juni Mosi, 2010, lilichapisha habari kwenye ukurasa wake wa kwanza chini ya kichwa cha habari, “Waziri Amuumbua Msemaji wa Rais”.

Katika habari hiyo, gazeti hilo lilidai kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Mheshimiwa Philip Marmo alikuwa amepingana na maelezo yaliyotolewa Mei 21, mwaka huu, 2010, na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu, kuhusiana na ziara za mawaziri nje ya nchi na katika mikoa mbali mbali nchini.

Katika taarifa yake ya Mei 21, mwaka huu, kwa vyombo vya habari, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilikuwa imekanusha habari zilizokuwa zimeandikwa na gazeti hilo hilo la Mwananchi chini ya kichwa cha habari, “Serikali Yahaha Uchaguzi Mkuu: Ikulu yazuia mawaziri kwenda nje, yawatuma mikoani kukutana na viongozi wa Dini na TUCTA’.

Ikulu imeshangazwa na kusikitishwa sana na kiwango cha juu cha jitihada na juhudi kubwa zinazofanywa na gazeti hili kufitinisha watu na kupotosha umma kwa jambo ambalo halipo, na inapenda kurudia na kusisitiza kama ifuatavyo:
  1. Siyo Ikulu wala Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewakataza mawaziri kusafiri nje ya nchi kama linavyodai gazeti hili. Hakuna waziri aliyezuiwa kusafiri nje.
  2. Siyo Ikulu wala Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza mawaziri kusambaa katika mikoa mbali mbali kukutana na viongozi wa Dini na TUCTA kama linavyodai gazeti hili.
Kama mawaziri wanakwenda mikoani kuelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya Awamu ya Nne ya uongozi wa Tanzania ni jambo jema. Na hiyo ni sehemu ya wajibu wao na kazi zao kama mawaziri wa Serikali. Na wala siyo wafanye hivyo kwa kutumwa ama kuagizwa na yoyote. Ni wajibu wao wa kikazi na uwajibikaji. Kama tulivyoelezea katika taarifa ya Mei 21, hakuna haja wala hoja ya msingi kwa Serikali kuwatuma Mawaziri ama hata watu wengine wowote kwenda mikoani kuzungumza na viongozi wa kiroho ama wale wa TUCTA. Kama wananchi watakavyokuwa wanakumbuka, mazungumzo kati ya viongozi wa dini na Serikali yamemalizika majuzi. Yalifanyika rasmi na hadharani pale Hoteli ya White Sands, mjini Dar es Salaam. Tena mazungumzo hayo yalikwenda vizuri na yalimalizika vizuri. Viongozi wa dini walifurahi sana.

Mazungumzo yenyewe yalifungwa na Mheshimiwa Rais Kikwete, na viongozi wa roho walifurahi kiasi cha kwamba wamependekeza kuwa utaratibu wa kuwa na mazungumzo ya namna hiyo liwe ni jambo la kudumu na yafanyike kila mwaka.

Na Mheshimiwa Rais Kikwete amekubali pendekezo hilo ambako sasa itafanyika mikutano miwili kati ya viongozi wa kiroho na wale wa Serikali kila mwaka. Mkutano mmoja utakuwa kati ya Serikali na kila dhehebu, na ule wa pili utakuwa kama ule uliomalizika White Sands yaani kati ya Serikali na viongozi wote wa kiroho.

Hivyo, kwa sasa Serikali haina sababu ya kuwatuma mawaziri wake kwenda kuzungumza na viongozi wa dini wakati mkutano kati ya pande hizo mbili umemalizika majuzi tu, tena vizuri, kwa kushirikisha viongozi wa kiroho kutoka mikoa yote.

Aidha, mazungumzo kati ya Serikali na TUCTA pia yamemalizika. Mazungumzo hayo yalimalizika Mei 8, mwaka huu, 2010, mjini Dar es Salaam. Haya nayo yalimalizika vizuri na pande hizo mbili zilikubaliana. Lililobakia sasa ni Serikali kuyafanyia kazi makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo kupitia taratibu na michakato mbalimbali ya Kiserikali ukiwamo mchakato wa Bajeti.

Sasa, kama mazungumzo kati ya Serikali na TUCTA yamefanyika vizuri na pande hizo mbili zimekubaliana, Serikali ama Ikulu, ina sababu gani ya kutuma mawaziri kwenda kuzungumza na viongozi wa TUCTA mikoani? Wanazungumza nini tena?

Hivyo, Ikulu inapenda kuwaambia wananchi kuwa kama ilivyokuwa kwenye habari ile ya Mei 21, habari ya jana ya gazeti hilo pia siyo ya kweli na ni ya kufitinisha watu na inastahili kudharauliwa na kupuuzwa.


Imetolewa na:


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.


02 Juni, 2010