Wednesday, October 6, 2010

Mkapa, Malecela, Sumaye wamkimbia Kikwete

VIGOGO waastafu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, wamekacha kampeni za mgombea urais Jakaya Kikwete, MwanaHALISI limeelezwa.
“Nakwambia kuna mgomo baridi ndani ya chama. Wastaafu wamekacha kampeni. Baadhi yao waligoma hata kuhudhuria siku ya ufunguzi wa kampeni,” amesema kiongozi mmoja wa chama hicho huku akitweta.
Amesema, “Hata wale waliokuja siku ya ufunguzi pale Jangwani, wengi walifika kutimiza wajibu tu, lakini ukweli ni kwamba wamesusa kampeni.”
Taarifa kutoka ndani ya CCM zinasema, uamuzi wa viongozi hao wastaafu unatokana na kile walichoita “Kikwete kuwa kichwa ngumu.”
Kwa mujibu wa taarifa za waliokaribu na viongozi wastaafu, hatua hiyo imefuatia Kikwete kushindwa kutekeleza maagizo na ushauri mbalimbali wa chama na viongozi hao.
Vigogo ambao wanadaiwa kukacha kampeni za Kikwete ni rais mstaafu Benjamin Mkapa, waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Mama Maria Nyerere na makamu mwenyekiti mstaafu, John Samwel Malecela.
Wengine wanaodaiwa kukacha kampeni ni rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salim Amour, mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba na katibu mkuu mstaafu, Philip Mangula.
Moja ya mambo yanayotajwa kutofurahisha wastaafu ni pamoja na serikali ya Kikwete kushindwa kupeleka bungeni muswada wa sheria ya “kutenganisha biashara na siasa” kabla ya uchaguzi mkuu mwaka huu.
Tangu mapema baada ya kuingia madarakani, Kikwete aliahidi kurejesha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na hasa maadili ya uongozi kwa jumla, katika serikali na chama chake kwa njia ya kutenganisha siasa na biashara.
Pamoja na kwamba Kikwete alilitaja hilo, ndani na nje ya mikutano ya chama, na hata kukaribia kujiapiza kuwa atalitenda, hakulitekeleza.
Jingine ambalo linatajwa kukasirisha wastaafu ni hatua ya Kikwete kuhamishia kampeni za uchaguzi katika familia yake.
Inadaiwa kuwa walioshika usukani wa kampeni za Kikwete ni mkewe, Salma na watoto wake, huku wakitumia rasilimali za umma.
Wakati Salma anazunguka nchi nzima kukutana na akinamama, Ridhiwani anazungukia vijana na baadhi ya wazee anakoelekezwa na baba yake.
Miraji Kikwete, mtoto mwingine wa Kikwete anadaiwa kushika mkoba wa fedha za kugharimia wasanii wanaozunguka na baba yake.
Sababu nyingine ambayo inadaiwa kuwakoroga wastaafu ni Kikwete kuendelea kumkumbatia Yusuf Makamba katika nafasi yake ya katibu mkuu.
Taarifa zinasema viongozi wastaafu walimtaka Kikwete kumwondoa Makamba katika wadhifa wake kwa maelezo kwamba hana uwezo wa kusimamia chama wakati huu wa uchaguzi.
Makamba amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wanachama, wabunge na wajumbe wa NEC, kwamba anavuruga chama na anatenda kinyume na maagizo ya vikao vya chama.
Bali kinachoelekea kuwastua wastaafu ni taarifa kwamba shughuli za chama zimehamishiwa mitaani Dar es Salaam badala ya kufanyika makao makuu madogo yaliyoko Mtaa wa Lumumba.
Mtoa taarifa ambaye ametaka jina lake lisitajwe gazetini amesema, Miraji anaendesha shughuli za baba yake kutoka ofisi iliyoko Mtaa wa Undali, Na. 175, Upanga, Dar es Salaam.
“Hapa ndipo imehamia timu nzima ya kampeni,” ameeleza mtoa taarifa.
Miongoni mwa watu ambao wameonekana wakiingia na kutoka kwenye jengo hilo la ghorofa moja, ni Mwenyekiti wa Kampeni, Abdulrahman Kinana, Katibu wa rais, Rajabu Luhwavi na Ofisa Habari wa kampeni za Kikwete, Muhingo Rweyemamu.
Wengine ni baadhi ya maofisa usalama wa taifa wanaofuatana na msafara wa Kikwete katika kampeni za uchaguzi na wengine wakiwamo wapigadebe wake wa mwaka 2005.
Ni katika jengo hili inadaiwa kituo kimoja cha televesheni nchini, kilifanyia mahojiano na Aminiel Mahimbo anayedai kuwa mke wake Josephine Mushumbusi “amechukuliwa” na mgombea urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Mwaka 2005 mtandao wa Kikwete ulihamisha shughuli za kampeni za urais kutoka Lumumba na kuzipeleka katika ofisi binafsi iliyokuwapo Mtaa wa Mindu, Upanga.
Inadaiwa ni katika ofisi hiyo, ilifanyika mipango ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) kupitia kampuni ya Kagoda na washirika wake.
Kuhusu kampeni kufanywa na chama, mtoa taarifa amemnukuu mmoja wa vigogo akisema, “Tulitaka kampeni zimilikiwe na chama…lakini hatukusikilizwa. Sasa mtandao wake hauheshimiki. Chama hakiheshimiwi. Badala yake kampeni ziko mikononi mwa familia,” anasema.
Chanzo chetu kilicho karibu na wazee hao kinahoji, “Sasa unataka wazee wastaafu waingie kama nani?”
Alipoulizwa Tambwe Hizza, Naibu Mkuu wa Idara ya Propaganda ya CCM, juu ya tuhuma za kuhamishia shughuli za kampeni mitaani alikiri, “Waliohamia huko ni watu wa IT - mawasiliano na habari tu - na si kwamba timu nzima ya kampeni imehamia hapo.”
Hata hivyo alisema “mambo yote yanafanyika hapa ofisi ndogo za makao makuu na hata hivi sasa ukija hapa utamkuta mzee Kinana akifanya shughuli za chama.”
Mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ambaye yupo karibu na Kinana ameliambia gazeti hili kuwa mwenyekiti huyo wa kamati ya kampeni ya Kikwete, amekataa kuhamishia shughuli zake mitaani.
“Mzee Kinana huwa anakwenda pale mara mojamoja lakini hajahamishia shughuli zake pale. Anaogopa yasije kutokea ya mwaka 2005 na halafu jina lake likachafuka kwa jambo asilolijua,” kimesema chanzo chetu cha habari.
Kuhusu kutenganishwa kwa siasa na biashara, mtoa taarifa anasema baadhi ya vigogo wastaafu wanadai kuwa kumekifanya chama kupitisha idadi kubwa ya wagombea ubunge na udiwani ambao ni wafanyabiashara na ambao hawafahamiki hata uadilifu wao.
Habari zinasema, tofauti na mwaka 2005 ambapo CCM ilijaribu kuchuja baadhi ya wafanyabiashara, katika uchaguzi huu, karibu ya asilimia 70 ya wanaogombea ubunge ni wafanyabiashara.
Mstaafu huyo ambaye hakutaka kutajwa jina anasema, “Kwa hali ya sasa, kusema chama hiki kinamilikiwa na wakulima na wafanyakazi ni kudanganya wananchi. Siwezi kushiriki katika kitu ambacho hata dhamira yangu inanisuta,” alieleza.
Aidha, kutoonekana kwa vigogo wastaafu kunahusishwa na jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wa sasa wamekuwa wakichukuliwa na chama.
Wakati kuna madai kuwa Mkapa analalamikia kuchafuliwa na baadhi ya wanamtandao wa mwaka 2005, Jaji Warioba amekuwa akitishiwa kupelekwa mahakamani, jambo ambalo linadaiwa kulenga kumchafua.
Vilevile Warioba amekuwa akidaiwa kumuunga mkono Dk. Salim katika kinyang’anyiro cha mwaka 2005; na mwaka jana alihusishwa na kuunga mkono maazimio ya kongamano la Taasisi ya Mwalimu Nyerere yaliyotaka rais achukue maamuzi mazito kurejesha heshima ya taifa.
Naye, Dk. Salim amekuwa majeruhi mkuu wa mtandao wa Kikwete. Katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005, ambapo alitwishwa zigo la tuhuma za kuwa mwarabu na kushiriki mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Kwa upande mwingine, Malecela anadaiwa kuchafuliwa wakati wa kampeni za kura za maoni jimboni mwake, kitu ambacho inadaiwa pia kiliandaliwa na baadhi ya viongozi ndani ya chama.
Phillip Mangula ni mhanga wa siasa za mtandao. Alitupwa nje mara baada ya Kikwete kuingia madarakani na baadaye kushindiliwa wakati wa kugombea uenyekiti wa mkoa ambapo alishindwa na diwani.
Kudondoka kwa Mangula kulifuatia Kikwete kukabidhiwa mikoba ya uenyekiti na mtangulizi wake, Benjamin Mkapa. Duru za gazeti hili zinamnukuu Kikwete akisema, “Leo hii usiku, Mangula si katibu mkuu tena wa CCM.”
Mangula aliibuka wiki iliyopita mjini Njombe kwenye mkutano wa kampeni za rais na kunukuliwa akisema amefurahishwa na uamuzi wa Kikwete wa kufanya Njombe kuwa mkoa.
kwa hisani ya saed kubenea wa mwanahalisi

No comments:

Post a Comment