Marehemu Moses Maira (Kushoto)Mwili wa wakili maarufu Moses Maira unatarajiwa kuwasili nchini leo usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi, KLM. Kwa mujibu wa wakili mwenzake, Mabere Marando, baada ya mwili huo kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam saa 6 usiku, utapelekwa nyumbani kwake Tabata. Kesho kutwa asubuhi, mwili utachukuliwa hadi Kanisa la Waadventista Wasabato Magomeni kwa ajili ya ibada maalumu kabla ya kupelekwa katika ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya heshima za mwisho. Baada ya hapo, Marando alisema, msafara wa kwenda katika makaburi ya Kinondoni kwa maziko utaanza ambapo anatarajiwa kuzikwa saa 9 alasiri. Maira (66) alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu iliyopita mjini Houston, Texas, Marekani, alikokwenda kutibiwa ugonjwa wa moyo na kisukari. Kabla ya safari yake ya Marekani, Maira alikuwa akimtetea aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Abdallah Zombe, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Dar es Salaam.Habari Kwa Hisani: Habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment