SERIKALI imeumbuka. Inahaha kukopa fedha benki kujazia bajeti, wakati inatuhumiwa kutumia mabilioni ya shilingi bila maelezo mwafaka.
Taarifa za kuaminika ambazo pia zinathibitishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinauweka utawala wa rais Jakaya Kikwete kitanzini.
Wakati serikali imekopa karibu Sh. 270 bilioni kutoka benki, CAG amethibitisha matumizi mabaya ya serikali yanayofikia Sh. 344.1 bilioni katika mwaka wa fedha uliopita.
Kiasi ambacho CAG anasema kimetumiwa vibaya au bila maelezo mwafaka, kinazidi fedha ambazo serikali inakopa kutoka benki kwa zaidi ya Sh. 74.1 bilioni.
Wiki iliyopita serikali ilisema imekopa Sh. 270 bilioni kutoka benki ya Stanbic ya jijini Dar es Salaam kujazia kwenye bajeti yake ya mwaka 2010/2011.
Hatua hiyo ya serikali inatokana na wafadhili kukata kiasi cha dola za Marekani 220 milioni sawa na Sh. 270 bilioni kutoka kwenye ahadi zao za kusaidia bajeti ya Tanzania kwa mwaka huo.
Wafadhili wameeleza kwamba kiasi hicho kimekatwa kutokana na serikali kutokuwa makini katika kukusanya mapato na kukosa nidhamu katika matumizi. Wameeleza kwamba serikali haitekelezi ahadi zake hasa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia kwa ujumla.
Kwa mujibu wa CAG, ofisi ya rais ni miongoni mwa zilizotumia vibaya fedha za serikali. Ripoti inaoyesha kuwa mwaka wa fedha wa 2008/2009 utumishi, iliyo chini ya ofisi ya rais, imetumia vibaya Sh. 282 milioni.
Fedha hizo zimetumika kulipia matumizi ya watumishi wake kulala hotelini, wakati watumishi hao tayari walilipwa na serikali fedha za kujikimu.
Aidha, CAG anasema ofisi hiyo imetumia kiasi cha Sh. 705 milioni bila ya kuwa na nyaraka za kuthibitisha matumizi yaliofanyika.
Katika kile kinachoonekana kuchota kila kinachopatikana, ofisi hiyo ya rais imelipa ofisa wake mmoja kiasi cha Sh. 13.3 milioni ikiwa ni asilimia 30 ya posho ya nyumba, huku akiwa amepewa nyumba na serikali.
MwanaHALISI lilipomuuliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo kuhusu matumizi ya ikulu na mengine ya serikali, alisema “ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.”
Alisema, “Sisi tumeipata ripoti hiyo ya CAG kwenye mkutano uliopita wa Bunge na bado hatujaidili. Kwa kweli katika mazingira haya nitakuwa napayuka tu kama nitazungumza lolote.”
Cheyo alisema sharti kamati yake ipate maelezo kamili ndipo iweze kutoa maoni yake.
Wizara nyingine ambazo CAG anasema zimetumia fedha vibaya au bila vielelezo sahihi, ni pamoja na wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi.
Katika wizara hiyo, CAG amegundua Sh. 3.6 bilioni zilizohamishwa kutoka fungu la matumizi ya kawaida kwenda katika fungu la ukarabati na manunuzi zilitumiwa vibaya.
CAG anasema katika ripoti yake kuwa, fedha hizo zilizohamishiwa fungu la ukarabati na manunuzi, hazikutumika kwa kazi iliyotajwa.
“…Hakukuwapo na ukarabati wala manunuzi yaliyofanyika. Mpango wa mwaka wa manunuzi na taarifa ya manunuzi, vilionyesha manunuzi hayo hayakufanyika kutokana na ukosefu wa fedha,” anasema CAG.
Matumizi mengine ya kutisha ni yale yaliyofanywa na wizara ya fedha yenyewe. Watendaji wa wizara hiyo, walipeleka kiasi cha Sh. 15 bilioni katika halmashauri mbalimbali ambazo hazikujulikana zilivyotumika.
Fedha hizo zimepelekwa bila ya kufahamisha Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) jambo lililosababisha “kutumika vibaya” au kuibwa, taarifa inasema.
Ripoti ya CAG inasema serikali ilitumia vibaya takribani Sh. 68 bilioni, ambazo hazikuwapo katika bajeti.
Aidha, serikali imetumia Sh. 23.7 bilioni ambazo zilitumia kuwekea dhamana Shirika la Umeme nchini (Tanesco). Shirika hilo lilishindwa kulipa deni lake na serikali ikalazimika kulilipa.
Lakini, kubwa kuliko yote, ni uamuzi wa serikali kubadili deni la Sh. 135 bilioni kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kuwa dhamana itakayolipiwa riba ya Sh. 11.50 kwa mwaka.
Kutokana na uamuzi huo, CAG anasema, “serikali italazimika kulipa kiasi cha Sh. 230 bilioni katika kipindi cha miaka 20 ijayo.”
Matumizi mengine ya Sh. 2 bilioni yamelipwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii inayomiliki kampuni ya M/S Pensions Properties Limited (PPL).
Mifuko hiyo imechotewa na serikali na washirika wake kiasi cha Sh 2, 845, 637,096 kama faini ya ucheleweshaji malipo yaliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa “ukumbi mdogo wa Bunge - Dodoma.”
Mifuko iliyolipwa fedha hizo ni Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF).
Kama hiyo haitoshi, CAG anasema serikali imelipa kiasi cha Sh. 4 bilioni kwa wamiliki wa hoteli ya Travertine ya jijini Dar es Salaam, kutokana na kushindwa katika shauri lililofunguliwa mahakamani na menejementi ya hoteli hiyo.
Menejementi ya Hotel Travertine ilifungua kesi Na. 350 ya mwaka 2002 kutokana na serikali kuvunja mkataba wake na hoteli ambao CAG anasema, “haukuwa na manufaa yoyote kwa serikali.”
Serikali pia imepoteza kiasi cha Sh 17.8 bilioni zilizokusanywa na Idara ya Uhamiaji Zanzibar ambazo hazikuwasilishwa katika serikali ya Muungano.
Ripoti hiyo imeeleza pia namna wizara ya fedha ilivyofanya manunuzi makubwa yenye thamani ya Sh 1.6 bilioni ili kuepuka fedha zilizokuwa hazijatumika hadi wakati huo zisirejeshwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari, wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alisema mapato ya serikali yameshuka kwa wastani wa asilimia sita.
Mkulo alisema Mamlaka ya Mapato (TRA) haikusanyi kama awali na uuzaji wa bidhaa nje umepungua.
Hata hivyo, Mkulo alijitetea kuwa uchumi wa nchi umeimarika kiasi cha kuwa na nguvu ya kukopa fedha hizo na kwamba hata washirika wa mawandeleo - Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) hawana kikwazo kwa maamuzi hayo.
Wakati Waziri Mkulo akipiga siasa katika suala nyeti la uchumi, taarifa zinasema sarafu ya taifa imeporomoka kwa kasi ambayo haijawahi kufikiwa.
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, sarafu hiyo imeshuka thamani yake kwa wastani wa Sh. 60.
Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu serikalini aliliambia MwanaHALISI kuwa ripoti ya CAG imeiumbua serikali, kutokana na mabilioni hayo ya shilingi kutojulikana yalivyotumika.
Katika Wizara ya Miundombinu, CAG amekutana na msururu wa madai ya wizara na idara za serikali zilizoagiza magari kupitia wizara hiyo, lakini yakiwa bado hayajafika.
Hata Ofisi ya Msajili wa Vyama imeguswa. Katika hali ambayo haijaweza kutosheleza ofisi ya CAG, msajili ametumia takribani Sh. 17 milioni kumlipia mtumishi wake mmoja fedha za kujikimu wakati wa mafunzo yake ya mwezi mmoja nchini Swaziland.
Kwa upande mwingine, CAG anasema wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imefanya manunuzi yenye thamani ya Sh. 103.06 milioni nje ya “mpango wa manunuzi wa mwaka” na bila manufaa.
Aidha, wizara ilitumia kiasi cha dola za Marekani 151,000 kukarabati jengo ililolinunua kwa dola za Marekani 10.5 milioni nchini Marekani, wakati kwa mujibu wa mkaguzi wa majengo, jengo hilo halikustahili kukarabatiwa. habari kwa hisani ya mwanahalisi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment