Sunday, June 20, 2010

Mwandosya ahujumiwa na wana CCM wenzake?


NYARAKA za siri zinazoonyesha mpango wa kumtokomeza kisiasa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya zimevuja.

MwanaHALISI limepata nyaraka hizo zinazomtaja mkuu wa mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa katika njama hizo.


Katika andishi rasmi, Mwakipesile anasema kwamba anatuhumiwa kushirikiana na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na swahiba wake mkuu, Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kumwangamiza Mwandosya kisiasa.


Profesa Mwandosya ni mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM). Alikuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye mchakato wa kugombea urais mwaka 2005.


Mwingine anayetajwa katika njama hizo ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mbeya, Nawab Mulla. Katika orodha hiyo, yumo pia mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa taifa, Cornel Apson Mwang’onda.


Kwa mujibu wa mawasiliano yaliyopo kati ya Profesa Mwandosya, Mwakipesile, Mwalimu wa Shule ya Msingi Lufilyo, Alisto Gideon Mwangungulu na Stephen Merali Mwakajumilo, wafadhili wakuu wa mkakati ni Rostam na swahiba wake Lowassa.


Taarifa zinasema Profesa Mwandosya huenda akagombea urais mwaka 2015, mwaka ambao pia imetajwa kuwa Lowassa angependa kuingia kwenye kinyang’anyiro.


Kuanguka kwa Profesa Mwandosya, taarifa zinaeleza, kunaweza kuwa ni kumsafishia njia Lowassa katika kuwania urais mwaka 2015.


Mwaka 2005 Profesa Mwandosya alikuwa mmoja wa wanachama wa CCM waliotoa ushindani mkubwa kwa rais Jakaya Kikwete katika kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais kupitia chama hicho.


Tangu wakati huo, taarifa zinasema, kumekuwa na madai ya kutaka kumuangamiza kwa maelezo kuwa anaweza kutamani kugombea tena nafasi hiyo mwaka 2015.


Aidha, taarifa zinasema Mwandosya amekuwa akikabiliwa na upinzani mkali kutoka ndani na nje ya chama, kutokana na kutokuwa mfuasi wa kundi maarufu la “wanamtadao,” lililomuingiza Kikwete madarakani.


Mkakati huo wa siku nyingi umevuja mwezi mmoja uliopita, baada ya Mwalimu Mwangungulu “kuungama” kwa Mwandosya akiwa na viongozi wengine wa dini.


Alisema aliitwa na Mwakipesile na kutakiwa kusaidia harakati za kumtokomeza Mwandosya.


Kwa mujibu wa mawasiliano ya siri kati ya viongozi hao wawili, Mwakipesile, anatuhumu Mwandosya kuwa mtu anayejisikia na asiyethamini viongozi wake wa mkoa na kitaifa.


Mwalimu Mwangungulu anasema katika ungamo lake kwamba Mwakipisile alimueleza, “…Mwalimu ngoja nikuambie yafuatayo: Mbunge wenu ana kiburi, ana dharau. Sijui ni kutokana na elimu aliyonayo?


Anasema, “…Nasema ana dharau na ana kiburi kwa kuwa akitoka Dar es Salaam anatakiwa kuripoti kwangu na wilayani. Yeye huwa anapitiliza moja kwa moja kwenda kijijini kwake Lufilyo.”


Mwangungulu alimnukuu Mwakipesile akisema, “Yeye (Profesa Mwandosya) amemwambia rais anihamishe kutoka mkoa huu, eti sina maendeleo yoyote.”


Alisema, “Mimi ndiye mkuu wa mkoa. Ndiye ninayepanga ratiba ya rais ya mkoa huu. Kwa hali hiyo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete hatakanyaga Lufilyo labda niwe marehemu au niwe nimehamishwa kutoka mkoa huu.”


Habari zinasema Mwakipesile aliona kuwa iwapo rais atakwenda kijijini Lufilyo, nyumbani kwa Profesa Mwandosya, basi waziri huyo angeweza kupata ujiko wa kisiasa.


Hata hivyo, Rais Kikwete alifika kijijini hapo mwaka jana baada ya kuombwa binafsi na Profesa Mwandosya wakati huo wakiwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani.


“Wakiwa Marekani (Mwandosya na Kikwete), Profesa alimuomba rais atembelee kijijini kwake kwa mwaliko wa mkewe, Mama Mark Mwandosya kwa ajili ya kufungua kituo cha watoto yatima cha Lufilyo. Ndipo Mwakipisile alipotaka kuhujumu ziara hii,” anasema kiongozi mmoja wa serikali aliyeulizwa iwapo anafahamu lolote kuhusiana na suala hilo.


Alisema, “Katika ziara yake ya kwanza mkoani Mbeya baada ya kurejea kutoka Marekani, viongozi wa mkoa hawakumpangia kutembelea Lufilyo. Lakini katika ziara ya pili, rais aliagiza kutoka Dar es Salaam, kwamba anakwenda Mbeya na anataka akifika tu, aende Lufilyo.”


Baada ya maelezo ya Mwangungulu, ndipo Profesa Mwandosya alipochukua hatua ya kumuandikia Mwakipesile kutaka kuweka kile alichoita, “kumbukumbu na matumizi ya baadaye.”


Katika barua yake ya tarehe 16 Aprili 2010, Profesa Mwandosya anasema, “…Naambatanisha kumbukumbu (transcript) ya kikao ulichokifanya (Mwakipesile, Mwalimu Mwangungulu na Mwakajumilo) Jumatatu ya Pasaka 3 Machi 2008 pale Mbeya Hotel. Somo la mazungumzo linajieleza lenyewe…ikiwa ni pamoja na washiriki wengine.”


Anasema kiini cha kupeleka kumbukumbu hizo zinazodaiwa kuandikwa na Mwalimu Mwangungulu, ni ili azipitie “na kufanya marekebisho” atakayoona yanafaa.


Barua ya Mwandosya kwenda kwa Mwakipesile ilikuwa na kichwa cha maneno kisemacho, “Kumbukumbu ya mkutano wa tarehe 3 Machi 2008.” Ilikuwa na Kumb. Na. MJM/JIMBO/RM/02.


Hata hivyo, Mwakipesile hakufanya marekebisho katika waraka wa siri aliotumiwa, badala yake aliandika barua ya kurasa mbili iliyojaa tuhuma, shutuma na lawama kwa Profesa Mwandosya.


Aidha, ni katika barua hiyo, Mwakipesile anaingiza hata watu ambao hawakutajwa mahali popote na Mwalimu Mwangungulu wala na Mwandosya.


Barua ya Mwakipesile ya tarehe 20 Aprili 2010 iliyotumwa kwa Profesa Mwandosya, kwanza inakiri kukutana na Mwalimu Mwangungulu na Mwakajumilo.


Mwakipesile anasema mkutano wao haukulenga kumuangamiza Profesa Mwandosya, bali kuzungumzia maandalizi ya semina ya SACCOS.


Akionyesha hasira katika maandishi yake, Mwakipesile anasema, “Nimeelezwa mengi juu ya masimango yako dhidi yangu, kwamba mimi John Mwakipesile nimemtafuta Mwakajumilo akuondoe ubunge.”


Anasema anadaiwa “…kupokea pesa kutoka kwa Lowassa na Rostam ili nikuondoea ubunge wewe na Mwakyembe. Kwamba mimi, Apson, Mwambulukutu, Mulla mwenyekiti wa CCM mkoa …ni adui zako ambao tuna lengo la kukuondoa uongozi na kuharibu malengo yako ya kisiasa. Unazungumza yote hayo na mengine mbele ya wananchi huko Mwakaleli ambao mimi ni kiongozi wao.”


Mwakipesile anasema, “Sitaki kuingia katika malumbano na wewe. Mimi bado nakuheshimu. Lakini sipendi kuniingiza katika mambo ya kijinga na ya kitoto.”


Akiandika kwa njia ya kumwonya Profesa Mwandosya, Mwakipesile anasema, “Nisingependa tena kuchezewa kiasi hiki.”


Wakati hali ikiwa tete katika jimbo la Mwandosya, Rhoda Mwamunyange, dada mkubwa wa mkuu wa sasa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Davis Mwamunyange, amekuwa mwanamke wa kwanza kujitosa kuwania ubunge katika jimbo la Kyela, mkoani Mbeya.


Rhoda ni mfanyakazi wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) jijini Dar es Salaam na mtumishi wa siku nyingi wa vyama vya wafanyakazi nchini. Jimbo la Kyela linashikiliwa na Dk. Harrison Mwakyembe.


Wengine wanaotajwa ni George Mwakalinga mjasiriamali na mwanafunzi anayeishi Uingereza na Vincent Mwamakimbula ambaye vilevile ni mjasiriamali anayeishi Dar es Salaam.


Habari kutoka jimbo la Urambo Mashariki zinasema Ali Karavina, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, ametajwa kujitosa kupambana na mbunge wa sasa, Spika wa Bunge, Samwel Sitta.


Mwingine aliyejitosa kupambana na Sitta ni Ali Kalimauganga.


Taarifa zinasema tayari “kadi feki” 36,000 zimeingiza jimboni humo. Haikufahamika nani ameziingiza, lakini Sitta alipoulizwa kwa simu kutoka Dodoma, alikiri kuwapo kwa kadi hizo na kusema kwa ufupi tu, “Sibabaishwi na majizi.”


Chanzo: Mwanahalisi

No comments:

Post a Comment